Home Kimataifa Barcelona inakwama wapi?

Barcelona inakwama wapi?

4199
0

Ukitazama jezi ya Barcelona kwenye sehemu ya ‘beji’ ya klabu kuna maneno ya kihispania ambayo tafsiri yake ina maana ya maneno haya ‘ZAIDI YA KLABU’ hii ni moja ya kauli mbiu ambazo zilibuniwa miaka hiyo iliyopita, kuitambulisha Barcelona kwa maana ya misingi na maadili yake vinaifanya kuwa zaidi ya klabu ya kawaida ambayo lengo lake ni kucheza soka.

Zaidi ya hapo Barca miaka ya karibuni imejijengea sifa ya kuwa klabu ambayo mara nyingi hutegemea vipaji ilivyovitengeneza yenyewe kwenye academy yake maarufu kama La Masia.

Dhana ya umaarufu wa La Masia ilijengeka tarehe 26, November miaka 7 iliyopita katika mchezo wa ligi ya Hispania dhidi ya Levante, katika dakika ya 14 ya mchezo huo mchezaji pekee wa Barca siku hiyo ambaye hakuwa na mizizi kwenye viwanja vya La Masia Dani Alves alitoka nje akiwa na jeraha na nafasi yake ilichukuliwa na Martin Montoya.

Mabadiliko hayo yalikuwa ya kihistoria kwani yalimaanisha kuwa kwa mara ya kwanza timu hii ilichezesha kikosi chote cha watu 11 ambao walianza maisha kwenye academy ya Barca na kufanikiwa kutoboa kwenye kikosi cha kwanza.

Miaka 7 ni mingi na leo ni mwaka 2019 hali imebadilika na La Masia ya leo haina tena Messi, Pedro, Busquet, Iniesta wala Xavi na matokeo yake imekuwa na sera ya usajili ambayo wanachama wa klabu hiyo wameshindwa kuielewa.

Hali hii ilithibitika kwa usajili wa kiungo mshambuliaji raia wa Ghana Kevin Prince Boateng ambaye amesajiliwa kwa mkopo toka Sassuolo ya Italia na endapo Barca wataridhishwa na uwezo wake watakuwa na fursa ya kumsajili kwa pauni milioni 7.

Yawezekana usajili wa KPB ukawa bahati mbaya lakini vipi kuhusu Paulinho, Arturo Vidal, wachezaji ambao kiumri hutegemei wakatajwa mwenye mipango ya muda mrefu ya klabu inayosifika kwa kulea na kukuza vipaji achilia mbali jinsi ambavyo Paulinho aliondoka na kurudi chini baada ya msimu mmoja au ambavyo Vidal anaonekana hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Ukiachana na hayo kuna kesi ya kipekee ya mtu kama Malcom ambaye alisajiliwa kwa style ya kumpoka mpinzani tonge mdomoni baada ya kumzuia kwenda AS Roma bila shaka winger huyo wa kibrazil anajutia kusaini Barca ambayo imemfahamisha kuwa January hii anaweza akaondoka.

Kuna mbrazil mwingine ambaye kuelekea tetesi za January ziliibuka kumhusu, Philippe Coutinho alisajiliwa kwa pesa nyingi lakini hadi tunavyozungumza hajajihakikishia nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.

Moja kati ya vitu vilivyoshangaza wengi ni namna ambavyo Barca walikubali kumuuza kwa haraka beki wa kimataifa wa Colombia Yerry Mina ambaye aliuzwa baada ya kujiunga toka Pelmeiras huku akiwa ameichezea Barca kwenye michezo isiyozidi mitano.

Kumuuza Mina inawezekana isiwe kitu cha ajabu lakini unapozingatia kuwa Barca wamepata wakati mgumu kwenye nafasi ya ulinzi msimu huu kutokana na Samuel Umtiti kukumbwa na majeraha na Gerrard Pique akiwa kwenye umri ambao hawezi kutegemewa kwa muda mrefu unagundua kuwa kulikuwa na ukurupukaji wa kiwango cha juu.

Katika uongozi wa Barcelona, moja kati ya watu waliojiunga na timu hii miaka ya karibuni ni Erick Abidal ambaye anashika anashika nafasi ya mkurugenzi wa ufundi na bila shaka moja kati ya majuku yake ni kuhakikisha anarejesha zama za La Masia ambayo iliogopwa.

Jukumu hili linaweza kuwa gumu kama hatazaliwa Messi mwingine au Iniesta na Xaxi, inapokuja suala la vipaji ambavyo Guardiola aliviona wakati akiwa na Barca B inawezekana Abidal asiwe na mengi ya kufanya lakini kwa usajili ambao Barca imekuwa ikiufanya kwa siku za karibuni kuna mengi ambayo anaweza kuyarekebisha hasa pale inapoonekana dhahiri shahiri hakuna mpango wa muda mrefu.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here