Home Kitaifa Maeneo matatu yatakayoamua ushindi hii leo Uganda vs Stars

Maeneo matatu yatakayoamua ushindi hii leo Uganda vs Stars

11733
0

Na Zaka Zakazi

Okwi vs Banda

Kukosekana kwa Kelvin Yondani kunamfanya Abdi Banda kuwa beki wa kati aliyedumu mfululizo zaidi kikosini.

Kocha Amunikie anapaswa kumtegemea beki huyo wa Baroka FC ya Afrika Kusini, kuongoza safu ya ulinzi sambamba na, aidha, Aggrey Morris au David Mwantika dhidi ya kinara wa safu ya ushambuliaji ya Uganda, Emmanuel Okwi.

Okwi ni mshambuliaji hatari na kwa kuwa anakutana na wachezaji anaowafahamu kutoka ligi aliyoizoea, TPL, anaweza akawa hatari zaidi.

Hupenda kutokea kushoto, akikatiza uwanja na kuingia ndani kutengeneza madhara. Lakini kwa kuwa Banda naye hutumia mguu wa kushoto, ni rahisi kumzuia Okwi.

Aucho vs Himid

Khalid Aucho na Himid Mao ni viungo wenye aina tofauti ya uchezaji.

Mao hutegemea zaidi utimamu wa mwili katika kutimiza majukumu yake uwanjani.

Ni kiungo wa chuma aliyekomaa zaidi katika siku za hivi karibuni hasa baada ya kujua kutofautisha ‘tough game’ na ‘rough game’.

Zaidi ya kusaidia kuziba mianya ya mipira kuelekea langoni mwake, Mao pia ana uwezo wa kusukuma mashambulizi mbele na kuisaidia upatikanaji wa mabao kwa kutengeneza nafasi au kufunga.

Aucho ni kiungo anayependa kupambana kwa hali na mali kuwafunika au kuwatoa mchezoni wachezaji kama Himid.

Hupenda kupiga chenga za maudhi na kubaki na mpira mguuni kumtamanisha mpinzani kucheza rafu, zitakazomsababishia kadi.

Himid akiweza kulidhibiti hilo, ataishinda vita hii…na akiishinda, Stars itatawala kiungo na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya ushindi.

Jjuuko vs Samatta

Mabingwa wa Tanzania, Simba SC, wamemuona Jjuuko Murshid kama ziada isiyohitajika kikosini mwao lakini kwa Uganda mlinzi huo ni lulu.

Dhidi ya Stars, Jjuuko atakuwa na kazi ya kuhakikisha nahodha Mbwana Samatta anakosa madhara au anakuwa na madhara madogo kwao, kama alivyomfanyia Mo Salah wa Misri.

Lakini hata hivyo, Jjuuko atakutana na Samatta tofauti kabisa kwani hakuna kipindi ambacho mshambuliaji huyo wa KRC Genk, amekuwa wa moto kama hiki.

Endapo Samatta ataweza kumkosesha raha Jjuuko, atatoka mchezoni na kuanza kucheza rafu ambazo zitamgharimu yeye mwenyewe…jambo ambalo ni faida kwa Stars.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here