Home Kitaifa MLIPUKO: Umri wa Okwi ni mwandiko wa daktari, ukiuchunguza sana utachanganya dozi

MLIPUKO: Umri wa Okwi ni mwandiko wa daktari, ukiuchunguza sana utachanganya dozi

28875
0

Unajua kwa sasa hakuna timu yenye uwekezaji mkubwa sana kuzidi Simba hapa Tanzania. Simba mpo vizuri. Mnafaa mpewe pongezi. Heko kwa Mo na Manara kwa kazi yenu kubwa.

Bila kigugumizi Simba imekamilika kila idara.

Nataka niwakumbushe kitu kidogo. Juzi Simba day wachezaji wenu walikuwa wanatambulishwa na kila mchezaji miaka yake iliwekwa wazi.

Nimeona watu mitandaoni wakiwa wanauliza au kuhoji hasa upi umri sahihi wa huyu mchezaji bora wa Uganda kuwahi kuchezea Tanzania kwa kipindi cha miaka takribani 10. EMMANUEL OKWI!

Mitandao mingi inaonesha Okwi amezaliwa Desemba 25 mwaka 1992.

Kimahesabu Okwi ana miaka 25 na sio kama ilivyobainishwa kuwa ana miaka 26 na Azam Tv wakati wa simba day.

Kwanini?

Kwa sababu kimahesabu tunasema Okwi alizaliwa 1993 kasoro siku 5 tu. Maana yake yake kila ifikapo desemba Okwi anatimiza mwaka na mpaka sasa sio desemba ni agost hivyo Okwi ana miaka 25 na siyo 26 ili tuende sawa.

Swali la Kujiuliza je yawezekana kweli Okwi akawa na umri huo?

Majibu ya moja kwa moja mimi sina. Nimejaribu kuchanganua mambo kadha wa kadha.

Kwanza Okwi ameanza lini soka
1.Sheria za kimkataba
2. Soka letu la Afrika
2.1. Miongozo ya mitandao n.k

Okwi alikuwa kijana mdogo wakati anapelekwa klabu ya wakubwa msimu wa 2007-2008. Kocha mkuu Paul Nkata ndiye aliyewapandisha vijana na kubeba ubingwa msimu wa 2008/2009 wachezaji vijana alikuwepo Emmanuel Okwi, Mike Azira, Tony Ndolo, Joseph Owino, Jeremiah Ssebuyira, Augustine Nsumba, Yusuf Juuko, Steven Bengo Yasin Mugabi, Oscar Kadenge, Godfrey Walusimbi.

Okwi msimu wake mwisho alimaliza na magoli 16 na kuisaidia klabu yake kutwaa ubingwa. Mwaka 2009 kimahesabu alikuwa na miaka 16 tu yaani hapa kwetu ni dogo wa kidato cha 3 au cha pili. Maana yake alianza ligi akiwa na miaka 14 au 15 mtoto wa kidato cha 2. Je inawezekana kweli kwa mtoto wa umri huo kucheza ligi kuu? Mimi SIJUI, maana hata kule ulaya watoto wanapokua kwa kasi sijawahi kuona au kusikia.

Je ni kweli na inawezekana tena ukiangalia hali ya maisha kwa hapa kwetu Afrika?

Nimejaribu kufuatilia takwimu zake Uganda ili kufanya ulinganifu sahihi wa umri wake.

Kwanza Okwi akiwa na miaka 14 alicheza ligi kuu Uganda. Ndio ni Machi 14 2007, Mchezo URA 0-4 Villa, nyakati hizo Villa ikiwa na nyota mkubwa Kadenge. Mchezo huo wafungaji ni [Oscar Kadenge 19, Stephen Bengo 56, Mike Azira, Emmanuel Okwi]. Yaani hapo Okwi kwa mujibu wa tarehe zake za kuzaliwa alikuwa na miaka 14 na miezi 3 ikimaanisha ni mtoto wa la saba aliyekuwa akisubiria matokeo yake ajue kama atakwenda kidato cha kwanza au lah kwa hapa kwetu.

Kushoto: Emmanuel Okwi, Mike Azira, Tony Ndolo, Joseph Owino, Simeon Masaba, Yusuf Juuko, Steven Bengo Squatting Kushoto chini: Yasin Mugabi, Oscar Kadenge, Godfrey Walusimbi Oscar Agaba

Picha juu Okwi hapo akiwa na aidha miaka 14 au 15. Kikosi hapo juu kilitawaliwa na vijana wengi wadogo.

Pili Emmanuel Okwi msimu wake wa mwisho alifunga bao dakika ya 27 kwenye mchezo wao dhidi ya KCC katika uwanja wao wa nyumbani mnamo agasti 2, 2008 akiwa na miaka 15, mabao yalifungwa na [Emmanuel Okwi 27; Vincent Kayizi 34, Patrick Ssenfuka 77] Villa wakipoteza mchezo huo nyumbani.

Sijaongeza chochote zaidi ya kutembea na takwimu zake za umri na mechi alizocheza.

Turudi nyuma. Nitawakumbusha taarifa moja ya hapo awali. Taarifa hii ipo kwenye ukurasa wa goal.com, Taarifa hii ilikuwa ya Edward Mbombay.

“Klabu ya Uganda ya SC Villa imemruhusu mshambuliaji wake tegemezi Okwi kuondoka na kujiunga na klabu ya Simba FC”

Pichani Okwi aliporejea Simba akitokea Sweden

Taarifa hii ni Julai 14, 2009 wakati huo kimahesabu Okwi alikuwa na miaka 16 na miezi na miezi 7 na siku 19.

Kwa takwimu za Wikipedia ambazo sio chombo cha kuaminika sana inaonekana Okwi aliichezea SC Villa michezo 40 na kufunga mabao 16 ya ligi pekee.

Tuendelee na suala la usajili wake.

Wakati Okwi anajiunga Simba wakati ule wachezaji wa URA Joseph Owino na mchezaji wa kimataifa wa Kenya Julius Owino walikuwa mbioni kujiunga na Simba FC.

“Sports Club Villa walikubaliana na miamba ya ligi kuu , Simba FC kwa ada ya $5000 ambayo kwa sasa unaweza kukadiriwa kufikia shilingi milioni 11 za Kitanzania (Ingawa zipo taarifa mbalimbali kuhusiana na ada yake ya uhamisho lakini hilo sio jambo la muhimu sana kwenye mada yetu). Yaani Simba ilinunua mchezaji huyo mwenye miaka 16 kwa kiasi hicho cha fedha ingawa kwa wakati huo sijui ilikuwa shilingi ngapi za kitanzania haswa”

Shirikisho la soka la Uganda FUFA, lilikamilisha fomu ya usajili kwa kuwa alikuwa mchezaji wa kimataifa (international transfer certificate (ITC)) kwa ajili ya Okwi kujiunga Simba.

Tunavyojua kuwa mchezaji haruhusiwi kucheza nje ya taifa lake kama hajafikisha miaka 18. Kuna taarifa zinadai kuwa Okwi hakuichezea Simba mpaka pale alipofikisha miaka 18. Kimahesabu Okwi angefikisha umri wa miaka 18 desemba 2011. Weka nukta hapa nitarejea.

Lakini shirikisho hilihili la FUFA chini ya mkurugenzi wake bwana Edgar Watson walisaini fomu ya ITC iliyomruhusu Okwi kusajiliwa chini ya shirika la mapato la uganda Uganda Revenue Authority (URA) pamoja na Joseph Owino huku wakijua wazi kuwa yule haruhusiwi kupewa kibali cha kufanya kazi nje ya nchi kutokana na Umri wake.

Narudi sasa pale nilipoweka nukta

Kuna taarifa zinazagaa mtandaoni kuwa eti Okwi alipojiunga Simba hakupewa nafasi kwenye kikosi cha kwanza alikwenda kikosi B mpaka pale alipotimiza miaka 18. Nimeshangaa sana taarifa hizi. Hawa hawa wanasahau kuwa Cliford Ndimbo alitaja kikosi cha wachezaji 26 huku Okwi jina lake likiwemo mwaka 2010 chini ya kocha Phiri aliyekuwa mpinzani mkubwa sana wa kocha Yanga Bwana Dusan Kondic.

Ni mwaka huo huo Emmanuel Okwi aliwafunga JKT Ruvu bao dakika ya 31 kwenye ushindi wa mabao 4 kwa 1 mnamo Oktoba 18 mwaka 2009 Okwi akiwa na miaka 16 na miezi 10. Mabao yalifuungwa na [Damas Makwayi 43; Uhuru Selemani 30, Emmanuel Okwi 31, Ramadhani Chombo 50, Mussa Hassan Mgosi 78]. Au mniambie mechi ya Simba dhidi ya JKT Ruvu mabao yalifungwa na nani?

Je sheria za FIFA hapo zinasemaje? Au naona Hili suala la kuhusu taratibu za FIFA tuachane nalo turudi kwenye mada yetu ya msingi tusije kufufua na mengine.

Taarifa zingine zinasemaje

Wikipedia inaonesha kuwa Okwi aliichezea SC Vila mechi 40. Lakini Wikipedia hiyo hiyo inaonesha kuwa Okwi alizaliwa mwaka 1987 lakini chini yake kidogo pia inasema Okwi alizaliwa 1992.

Mantiki yangu ni nini? Je nina wivu na Simba? Je namchukia Okwi? Je maelezo yangu sipo sawa? Hapana.

Narudi kwa wadau wa soka. Tuweni makini sana katika masuala ya umri wa wawachezaji bila kuangalia usoni. Hao mnaowaita maskauti wawe makini katika kumjua mchezaji vyema. Inawezekana waganda wametupiga changa la macho lakini Simba bila kujihakikishia taarifa zao wakaingia mkenge. Nawaza tu.

Najua wapenzi wa Simba watanijibu shida sio umri shida ni kipaji. Sawa lakini athari zake kwenye ukuaji wa soka letu si nazijua lakini?

Hapa kuna mawili labda taarifa za mitandaoni ni za upotoshwaji na Simba wanataarifa kamili tofauti na hizi.

Lakini kumbukeni Emmanuel Okwi ameitwa timu ya taifa ya Uganda 2009 akiwa na umri wa miaka 16 na miezi miwili kwa mujibu wa transfermarket na mchezo wake wa kwanza wa mashindano alicheza uwanja wa Nyayo kule Kenya kwenye mechi ya Cecafa dhidi ya Rwanda (2-0). Kwa hiyo inawezekana hizi taarifa za yeye kuzaliwa 1992 ni za kweli licha ya kwamba mimi napata ukakasi.

Kama kuna upikwaji wa taarifa hizi basi hii inatengeneza picha mbaya kwa soka letu, inahamasisha ujanja ujanja wa kufoji vyeti n.k. sitoshindwa kulisema hili kwa sababu ni Simba au ni Yanga hapa. Aidha hoja hizi zijibiwe kama viongozi wa Simba wataona hili au viongozi wa Simba wafunike kikombe mwanaharamu nipite lakini mwisho wa siku wajichunguze. Najua nimepiga mzinga wa nyuki jiwe. Sijamhukumu Okwi ila nimeongelea sakata hili kwa mujibu wa mitandao huenda mitandao inapotosha hivyo tungeomba Manara atupe majibu na sio mapovu.

Lakini hata hivyo tusishangae sana kuhusu mchanganyiko wa umri wake maana hata Raisi wa Uganda hivi majuzi tu palitokea sintofahamu ya umri wake hii ndio Afrika. Kama Okwi ana miaka 25 maana yake ana miaka 10 ya kucheza ili kufika umri wa Buffon au Iniesta. Tehe tehe

Ila hii Simba noma sana. Makombe kama yote. Hadi wazungu wamesema moto wao hauzimwi na magari labda zije ndege za zima moto.

Imeandikwa na Privaldinho (Instagram)

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here