Home Kimataifa Okwi anapendwa na mashabiki, Bwalya anapendwa na magoli

Okwi anapendwa na mashabiki, Bwalya anapendwa na magoli

9632
0

Kumwachia Okwi aondoke wakati huu mhh na kutegemea makubwa klabu bingwa ni sawa na kuchoma mahindi na tochi.

Sijui mtawaaminisha vipi mashabiki wa Okwi ambao wakati Okwi anazomewa mhenga wala hawakujali makelele ya umri wake.

Mashabiki hawataelewa kabisa watahisi kuwa huu uamuzi ni wa kinyemela. Wakati fulani kuzuia riziki ya mtu ni uchawi. Kaizer Chiefs sio timu ndogo. Nina uhakika wameweka donge kubwa sana kumpata Okwi (kama taarifa hizo ni za kweli). Sio timu ya njaa njaa na huenda maslahi ya Okwi pia ni makubwa.

Hii ni ofa kubwa sana kwake hasa katika umri wake wa kwenye passport. Wakati fulani ni heri fedheha kuliko lawama. Itakuwa lawama kubwa sana kama Okwi atanyimwa kuondoka na sidhani kama Mo ana roho ngumu kiasi hiki.

Kikubwa ni maslahi ya mchezaji cha pili maslahi ya klabu. Yamkini Okwi ndiye aliyeomba kwenda, je kwanini mtoto aombe samaki tumpe jiwe?

Kama Okwi ataondoka Simba wanahitaji utulivu wa hali ya juu kuziba pengo lake. Wawe makini sana isije ikawatokea ule mzimu wa namba 7 pale Ugani Old Trafford. Nimesikia tetesi kuwa Walter Bwalya kuwa anakuja Simba. Binafsi kwangu Walter Bwalya ni usajili sahihi zaidi ambao Simba nahisi kama utafanyika kwa wakati muafaka.

Bwalya ni Monsta. Ni jini. Ni mtu mbaya. Bwalya analijua goli huenda hata kuliko mchezaji yeyote wa kibongo au anayecheza hapa bongo.

Hivi majuzi mwezi januari USM Alger ilitaka kunasa huduma zake kwa Takribani Milioni 500 za Kitanzania lakini wakashindwana kwenye masuala binafsi. Huyu Bwalya ni watu watatu na robo. Yaani uchezaji wake na uwezo wake wa kuliona lango ni hatari mara kumi elfu. Watakaomfananisha Bwalya na wachezaji wetu hawa wa ndani basi ni sawa na kukonyeza huku umevaa miwani.

Bwalya ni raia wa Kongo, Kinshasa. Ana miaka 25. Hivi majuzi alishutumiwa kwa kashfa za uchakachuaji kuhusu uhalisia wa uraia wake.

Historia yake kwa ufupi

Alipotua Nkana akitokea Forest Rangers mwaka 2015 msimu wake wa kwanza 2014 alifunga magoli 7. Goli lake la pili kwenye historia ya ligi kuu Zambia alilifunga dhidi ya Zesco ugenini na kuipa Forest Ushindi mnamo June 14 2014. Dirisha dogo la usajili akasajiliwa kwa mkopo na Nkana ambapo kwa mara nyingine tena aliifunga Zesco bao moja dakika 49 lakini zamu hii Nkana walikufa bao 5-3 mnamo August 15. Baadae Sept 15 aliifunga timu yake ya zamani ya Forest bao 1 na kuipa Nkana ushindi wa goli 1-0.


Msimu wa 2016 alichukua kiatu cha mfungaji bora kwa mabao 24 tena akiongoza ufungaji kwenye zile ligi bora 8 Afrika.

Algeria – Mohamed Zubya 13 Magoli
Africa Kusini – Collins Mbesuma 14 Magoli
Kenya – John Makwata 15 Magoli
Misri – Hossam Salama 17 Magoli
Ghana – Latiff Blessings 18 Magoli
Nigeria – Godwin Obaje 18 Magoli
Tanzania – Amissi Tambwe 21 Magoli
Zambia – Walter Bwalya 24 Magoli


Wakati Bwalya anabeba kiatu cha ufungaji alimpita namba mbili Jesse Jackson kwa idadi ya magoli 9. Mara ya mwisho mfungaji bora Zambia kumaliza msimu na magoli zaidi ya 18 ilikuwa mwaka 2009 ambapo Patrick Kababa alipomaliza msimu na magoli 20.

Msimu uliofuata 2017 kutokana na matatizo ya uraia wake mzunguko wa kwanza alicheza idadi ndogo za ya mechi na mzunguko wa pili alitia kimyani magoli 12.


Takwimu zake kwa mujibu wa rsssf na Zambianreports
2014 – 2015: Magoli 7
2015 – 2016: Magoli 24
2016 – 2017: Magoli 12
2017 – 2018: Magoli 10


Ndani ya miaka 4 tayari ana magoli 53. Akiwa na umri wa miaka 25 tu. Je kuna sababu ya kumbeza? Shida ninayoiona hapa, itabidi Bwalya asubiri mpaka mwezi wa 8 ili acheze ligi kuu na michuano ya klabu bingwa (Cup tied)! Hii ni hasara kwa Simba na kiwango cha Bwalya pia. Bwalya hataruhusiwa kucheza klabu bingwa lakini hatoruhusiwa kucheza ligi kuu.

Hii nayo ni changamoto. Kuna mengi ya kufanywa hapa, aidha kuweka oda mapema au kusubiri mpaka dirisha lifunguliwe.

Kama kweli Okwi ataondoka basi Bwalya ndiye mtu sahihi.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here