Home Ligi EPL Sarri ametuonyesha umuhimu wa kupaki basi

Sarri ametuonyesha umuhimu wa kupaki basi

8732
0

Kuna watu wanamsema sana Mou na mfumo wa kukaba. Sijajua nani kaawaambia huo mfumo haufanyi kazi?

Kuna watu wameponzwa na aina ya uchezaji wa timu fulani fulani wakiamini kuwa timu nzuri ni ile inayocheza pasi.

Mfumo wa kukaa nyuma na kukaba ni moja ya mfumo mgumu kuutumia kama huna wachezaji wanaojielewa. Siyo mfumo mrahisi hata kidogo. Wala haujapitwa na wakati kama wengi wanavyodhani.

Kwenye soka hakuna mfumo wa zamani wala wa kisasa. Kinachobadilika ni aina ya wachezaji unaokuwa nao. Mfumo wa pasi nyingi ulikiwepo tokea zamani. Haujaanza leo. Kupaki basi upo tokea zamani Haujaanza leo.

Tazama mechi ya leo chelsea wamezidiwa karibia kila kitu ispokuwa magoli.

UMILIKI
Chelsea: 38%
City: 61%

(Yaani Laporte na Stones walipiga karibia nusu ya pasi zote walizopiga Chelsea. Chelsea wamepiga pasi 411 Wakati Stones na Laporte wamepiga jumla ya pasi 207.)

MASHUTI
Chelsea: 8
City: 14

KONA
Chelsea: 1
City: 14

Chelsea walionekana kukaba zaidi kuliko City.

Chelsea wameondosha hatari katika eneo lao mara 101 huku City wakifanya hivyo mara 53 tu. Ni dhahiri kuwa Chelsea waliwekeza zaidi kukaba. Chelsea walicheza kwa tahadhari kubwa sana. Walifanya mashambulizi ya kushtukiza sana. Kabla ya kupatikana kwa bao la N’golo Kante Chelsea walifanikiwa kupiga pasi 18 katika robo ya eneo la ulinzi wa City. Muda mwingi Chelsea walikuwa nyuma kujilinda.

Katika mchezo mzima Chelsea walifanikiwa kufika robo ya sehemu ya ulinzi ya wapinzani wao kwa kupiga pasi 54 tu huku City wakipiga pasi 184 katika eneo la ulinzi la Chelsea.

Chelsea walitumia mbinu ya kuuficha mpira katika eneo lao zaidi kwani katika pasi 411 walizopiga pasi 169 walipiga katika robo ya eneo lao la ulinzi. Hata hivyo eneo la katika lilikuwa gumzo katika mchezo wa leo kwani hakukuwa na uchochoro kabisa katika eneo hilo. Sio Fernandinho, Kante au Jorginho aliyepwaya kwani hakuna pasi iliyopigwa eneo la katikati kuelekea lango la madui iliyozaa matunda au kufika.

Ni pasi moja tu iliyokamilika katika mchezo mzima kutokana na uzito wa ngome zote. Mchezo huu ulitawaliwa na mipira mingi ya krosi baada ya vita ya viungo na mabeki wa kati kuwa nzito.

Chelsea krosi 6 na Man City wakapiga krosi 23.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa.

Mpira una njia zake. Mpira ni malengo na mipango. Sio pasi au visigino, kanzu na udambwidambwi. Mpira ni sayansi. Ukichanganya vibaya kemikali zako unajikuta unaunguza maabara

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here