Home Ligi EPL Yaliyomkuta Mourinho amejitakia mwenyewe

Yaliyomkuta Mourinho amejitakia mwenyewe

4436
0

Maisha yanabadilika mazingira mpaka tabia, nchi zimebadili mengi na sasa tabia maisha zimeibuka, kasi ya mabadiliko imekuwa kubwa na hakuna tena anayetaka kuishi kwenye wakati uliopita kila mtu anasonga mbele.

Tizama jua likiwa katika mzunguko wa mawio na machweo na utaona halijabadili mwendo au aina ya uzamaji na uibukaji lakini wapo binadamu watakwambia jua limebadili tabia kabisa, maisha hayafanani na usiku unakuwa mfupi kuliko mchana siku hizi.

Binadamu mmoja anaweza kuwa Jose Mourinho mwite The Special One, huyu ambaye alikuwa na kiburi kwa sababu aliamini yeye ni bora, huyu ambaye alikuwa jeuri kwa sababu siku zote alikuwa mshindi na huyu ambaye alikuwa maarufu kwa sababu dunia aliiweka katika viganja vyake.

Katika kizazi chake Mourinho aliweza kujenga jeshi popote alipokwenda na alifanikiwa kushinda vita kubwa nyingi ambazo ni kuanzia EPL, Serie A, La Liga na bila kusahau maajabu yake na Porto, huyu alikuwa Mourinho mwanaume wa shoka!

Mourinho aliondoka pale alipojisikia na aliondoka wakati anahitajika hata kama alikosana na wamiliki. Mabadiliko ya tabia ya soka yamefika kama ilivyokuwa tabia ya nchi na sasa kwenye nyuso za Mourinho muda mwingi kulikuwa na sura ya Twiga mpoole badala ya uchui aliozowesha kuwatisha watu.

Akiwa amefanikiwa kutwaa mataji kama Carabao, Europa League na Ngao ya Jamii kwenye misimu yake miwili ya kwanza, msimu uliopita pia amemaliza katika nafasi ya pili, wengi walitegemea huu ungekuwa msimu wake wa mapambano.

Hakuna kilichobadilika kwenye kikosi chake kilichopita kwa maana ya wachezaji kupungua bali aliweza kuongeza wachezaji walioletwa kwa gharama kubwa iwe usajili ama mshahara kama Alexis Sanchez na kiungo Fred.

Wapo wanaoamini kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa klabu hiyo Ed Woodward anastahiki lawama, ndiyo anaungana nao mkono kabisa kwa sababu Mourinho alihitaji kushindana kutwaa ubingwa kwa kupata beki aliyemuhitaji.

Hata hivyo inawezekana ikawa haihitaji sayansi kubwa kushangaa inakuwaje leo hii safu ya ulinzi inayoruhusu mabao 28 kwenye michezo 38 ya msimu uliopita iwe imeruhusu mabao 29 kwenye michezo 17 tu mpaka sasa.

Hii ni ajali mbaya na iliyobeba maana kubwa, United ilikuwa kwenye kasi ya kumaliza msimu ikiwa imefungwa magoli 65 yaani magoli 36 zaidi ya msimu uliopita.

Kama hiyo haitoshi, safu yao ya ushambuliaji ilishuka ingeweza kufunga mabao matatu au pungufu ya msimu uliopita kwa maana ya mabao 65 dhidi ya 68 waliyofunga msimu uliopita.

Mchezaji wao bora David De Gea alikuwa na wastani bora zaidi kuokoa michomo iliyoelekezwa golini lakini amekuwa msimu mbaya zaidi kwa sasa tafsiri yake ni kuwa timu haina morali.

Inawezekana bahati mbaya zaidi ni kuwa wakati uliopo una Sarri, Pochetino, Unai Emery, Klopp na Guardiona wanaishi chini ya wingu moja na jua linalowachoma linashabihiana, hawa wanafanya maisha ya Mourinho yawe magumu zaidi kwa namna walivyojipanga.

Kuna tatizo moja kwa Manchester United ambalo litadumu kwa muda kiasi nalo ni Ferguson huyu aliifanya Old Trafford kwa mbaali ionekane Paradiso, alihakikisha kila binadamu anaepumua haishi kutamani kuangukia pale. Mourinho alifika akiwa na ndoto ya muda mrefu ya kumrithi Ferguson lakini badala yake alikuwa anarithi klabu ya Ferguson ambayo ilikuwa imepitia falsafa tatu tofauti katika kipindi kifupi.

Wapo wachezaji walioishi maisha ya Fegie wakazaliwa na Moyes kisha zikaja mbinu za Van Gaal na baadaye zote alitakiwa kuzibadili ziendane naye. Nilikuwa naandika hapa naungana na Garry Neville kuwa kosa pekee la Ed Woodward kama aliamini kuwa hatompa fedha nyingi Mourinho ilikuwa ni kumpa mkataba mpya wakati akifahamu fika Mourinho hajawahi kuwa na misimu mitatu bora kwenye klabu alizopitia.

Mourinho aliwakosea mashabiki kwa kushindwa kuonesha kuwa timu ilihitaji na ilipigania ushindi msimu huu na Ed Woodward aliikosea Manchester United kwa kushindwa kufanya maamuzi sahihi ya kuachana na Mourinho mapema au kutoa fedha nje ya kiwango alichotakiwa.

Kuna swali moja pekee na gumu zaidi ambalo sioni linamtoaje Mourinho kwenye lawama za kushindwa kutumia wachezaji wake Alexis Sanchez, Paul Pogba, Fred na Romelu Lukaku wote ni wachezaji aliowanunua kwa fedha nyingi zaidi na wote wameshindwa kuonesha uwezo wao chini yake.

Sasa hawa wote ni tatizo la Woodward? Au wakati ndio umeshamuacha ndugu yetu Mourinho.

Comments

comments

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here